4 Desemba 2020 - 19:01
Khatibzadeh: Uhawabi ndio chimbuko la chuki na ugaidi katika eneo na nje yake

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, makundi yote ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi yamepewa mafunzo ya elimu katika madrasa zinazofadhiliwa kifedha na Saudi Arabia.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Saeed Khatibzadeh ametoa kauli hiyo kujibu madai ya waziri wa nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia aliyotoa dhidi ya Iran.

Adel al-Jubair alisema hivi karibuni katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, mwenendo wa Iran umesababisha watu wengi kuuliwa nchini Saudia.

Khatibzadeh amesema kuhusiana na madai hayo ya al-Jubair kwamba: Kwa miongo kadhaa, Uwahabi uliolelewa na madola ya kikoloni ndilo chimbuko pekee la taasubi pofu, chuki na ugaidi katika eneo la Asia Magharibi na nje yake.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, kiwango chochote cha uzushaji utata unaofanywa na Wasaudi hakiwezi kuficha ukweli huo ulio wazi; na jinai za Yemen na faili chafu la mauaji ya Jamal Khashoggi ni baadhi ya vituko vya maovu yao wanayofanya.

Saeed Khatibzadeh amesema, kituko cha karibuni kabisa cha Wasaudi ni cha kusimama bega kwa bega na mfadhili mkuu wa ugaidi wa kiserikali, yaani utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina na akasisitiza kuwa, sera za kuchochea na kuzusha mivutano haziwezi kudumu tena na inawapasa Wasaudi wabadilishe mwenendo wao huo.../

342/